Exodus 2

Kuzaliwa Kwa Musa

1 aBasi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, 2 bnaye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. 3 cLakini alipoona hawezi kumficha zaidi, akamtengenezea kisafina cha mafunjo, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha katikati ya matete kando ya ukingo wa Mto Naili. 4 dDada ya huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto.

5 eNdipo binti Farao akateremka mtoni Naili kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti mfalme akaona kisafina katikati ya manyasi, akamtuma mmoja wa watumwa wake wa kike kukichukua. 6Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Kiebrania.”

7Ndipo dada wa huyo mtoto akamuuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Kiebrania akulelee huyu mtoto?”

8Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. 9Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. 10Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”

Musa Akimbilia Midiani

11 fSiku moja, baada ya Musa kukua, akaondoka kwenda walikokuwa watu wake, na akachunguza jinsi walivyokuwa wakifanya kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmojawapo wa watu wake. 12Musa akatazama huku na huko asione mtu yeyote, akamuua yule Mmisri, akamficha mchangani. 13 gKesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamuuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?”

14 hYule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekufanya mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri?” Ndipo Musa akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”

15 iFarao aliposikia jambo hili, alijaribu kumuua Musa, lakini Musa akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima. 16 jKuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza hori kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao. 17 kBaadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Musa akainuka, akawasaidia na kunywesha mifugo yao.

18 lHao wasichana waliporudi nyumbani kwa Reueli baba yao, akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?”

19Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikononi mwa wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.”

20 mAkawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.”

21 nMusa akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Musa binti yake aliyeitwa Sipora amwoe. 22 oSipora alizaa mtoto wa kiume, naye Musa akamwita Gershomu, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”

23 pBaada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu. 24 qMungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka Agano alilofanya na Ibrahimu pamoja na Isaka na Yakobo. 25 rKwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.
Copyright information for SwhKC